

Lugha Nyingine
Wataalam waeleza manufaa ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja kwa nchi za Pembe ya Afrika
Mhariri Msaidizi wa Gazeti la Eritrea Profile, Sirak Habtemichael akiwa na waandishi wenzake wa kimataifa wanaohudhuria Baraza la Tatu la Ushirikiano wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI). (Picha kutoka mhojiwa)
Mihrete Tiruwork Ayalew (kushoto), Mhariri wa Shirika la Habari la Ethiopia akiwa katika mahojiano na Aris, mwandishi wa People’s Daily Online. (People’s Daily Online)
Mwandishi wa habari mwandamizi kutoka Somalia, Tahir Abdallah katika mahojiano na People’s Daily Online. (People’s Daily Online)
BEIJING - Nchi za Pembe ya Afrika zimepata manufaa mengi halisi na yanayoonekana kutokana na ushirikiano wa ujenzi wa pamoja wa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja hasa katika nyanja za miundombinu, mabadilishano kati ya watu na ya kitamaduni, ujengaji wa uwezo na uhamishaji wa teknolojia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mahojiano na People’s Daily Online, wataalam na waandishi wa habari kutoka nchi za Ethiopia, Somalia na Eritrea ambao wapo Beijing, China kuhudhuria Baraza la Tatu la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja wamesema, maendeleo hayo yamesaidia sana kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kusaidia kupunguza umaskini miongoni mwa watu katika nchi husika.
Mihrete Tiruwork Ayalew, Mhariri wa Shirika la Habari la Ethiopia amesema nchi yake ya Ethiopia inafanya vema sana katika pendekezo hilo, huku akisema, Ethiopia ina miradi mingi ya ushirikiano chini ya BRI katika sekta mbalimbali kama vile elimu, nishati, viwanda na uchukuzi hususan ujenzi wa reli ya kisasa inayounganisha Ethiopia na nchi jirani ya bahari ya Djibouti.
Akizungumzia mradi huo wa reli ambao amesema ni mkubwa zaidi na wa kihistoria uliojengwa kwa ushirikiano wa China, Ethiopia na Djibouti, Ayalew amesema unaipa Ethiopia, nchi isiyo na habari ufikiaji wa bandari, ina mchango mkubwa kwa usafirishaji wa watu na uchukuzi wa bidhaa na kusaidia kustawi kwa biashara ya ndani na ya nje ya Ethiopia.
“Reli hii ina mchango mkubwa kwa Ethiopia katika kuuza na kuagiza bidhaa nje kwa sababu tunatumia bandari ya Djibouti, Ethiopia inasafirisha bidhaa na mazao mengi ya kilimo duniani” amesema Ayalew.
Naye Mhariri Msaidizi wa Gazeti la Eritrea Profile, Sirak Habtemichael amesema nchi yake ya Eritrea ilisaini makubaliano ya BRI Mwaka 2021 na tangu wakati huo nchi hiyo imepata manufaa mengi ikiwemo kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, ujenzi wa miundombinu, uhamishaji wa teknolojia na mabadilishano ya utaalam hususan katika sekta za elimu na afya.
Amesema hata kabla ya kuwepo kwa BRI nchi yake tangu ipate uhuru Mwaka 1993 imekuwa na historia ndefu ya ushirikiano na China huku akisema maendeleo mengi yamepatikana katika miundombinu, mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi ya pande mbili na uwekezaji wa kampuni za China katika sekta mbalimbali kama uchimbaji madini.
Kwa upande wake Tahir Abdallah, mwandishi wa habari mwandamizi kutoka Somalia amesema, BRI imekuwa wazi kwa nchi mbalimbali kushiriki. Kwa nchi za Afrika, hasa katika pembe ya Afrika pendekezo hili linatekelezwa kikamilifu katika nchi karibu zote akitolea mfano Ethiopia na Djibouti.
“Kumekuwa na ushirikiano zaidi, miradi mingi mipya zaidi, biashara zaidi ambavyo kwa pamoja vimeleta manufaa kwa pande zote mbili zinazoshiriki” amesema Talik ambaye yeye na wenzake wamekuwa hapa China tangu Julai mwaka huu kushuhudia hatua mbalimbali za maendeleo zilizopigwa na China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma